Mabadiliko ya huduma za Kampuni ya Ndege Tanzania-ATCL (8)

Jafari Juma, Mwananchi

Mpendwa msomaji wa safu hii ya mabadiliko ya huduma za Kampuni ya Ndege Tanzania, karibu katika muendelezo wa makala hizi ambazo zinazungumzia mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika kampuni hiyo.

Kwenye toleo la makala iliyopita tuliangalia awamu ya kwanza ya mpango wa upanuzi wa mtandao wa ATCL ambapo tulizungumzia kuhusu mpango wa kupanua huduma za kampuni hiyo uliyohusisha mambo yafuatayo.

Kuimarisha huduma za ATCL

Jambo la kwanza kufanyika katika awamu ya kwanza ya mpango wa upanuzi wa huduma za ATCL ilikuwa ni kuimarisha huduma za kampuni ili iweze kutoa huduma iliyokamilika hapa nchini kwa kuongeza viwanja, kwa sababu kabla ya hapo ndege za ATCL zilikua zinaenda viwanja vinne pekee ambavyo ni Tabora, Kigoma, Mwanza na Comoro.

Kupanua mtandao wa ndani

Katika mpango huu, kampuni hiyo iliweza kuongeza viwanja vya ndege ambavyo ndege za kampuni zilikuwa hazifanyi safari zake, viwanja hivyo ni pamoja na Zanzibar na Kilimanjaro. Pia kampuni hiyo iliongeza miruko katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Bukoba, Tabora, Dodoma, Songea, Mtwara, Mbeya, pamoja na Comoro.

Upanuzi huu ulihusisha pia ongezeko la wafanyakazi, wahudumu pamoja na ndege ili kuweza kutoa huduma iliyokamilika kwa wananchi. Lengo la kupanua mtandao wa ndani ni kutengeneza mtandao wa kutosha kwa ajili ya maandalizi ya kuanza safari za kwenda nje ya nchi.

Hivyo awamu hii ilihusisha kurudisha safari za ATCL kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini pamoja na kuongeza miruko ya ndege za kampuni katika viwanja ambavyo ndege za kampuni hiyo zilikuwa zinakwenda awali.

Baada ya kukamilika kwa mpango wa upanuzi wa huduma za ATCL awamu ya kwanza, kampuni hiyo ilianza utekelezaji wa upanuzi wa huduma hizo kwa wamu ya pili ambapo awamu hiyo ilihusisha upanuzi wa mtandao wa ATCL nje ya Tanzania.

Katika awamu hii ATCL ilianza kufanya safari za Dar es Salaam kwenda Entebbe (Uganda) na Dar es Salaam kwenda Bujumbura (Burundi). Aidha mwezi Februari mwaka huu kampuni hiyo inaanza safari za kutoka Dar es Salaam kwenda Harare (Zimbabwe) pamoja na Dar es Salaam kwenda Lusaka (Zambia).

Pia, katika kupanua mtandao wa ATCL nje ya Tanzania, kampuni hiyo iko mbioni kuanzisha safari za Johannesburg (Afrika Kusini), Mumbai (India), Hong Kong, Thailand pamoja na Guangzhou (China).

Kutokana na maandalizi yaliyofanyika mpaka sasa kwa ajili ya kuanzisha safari hizo, kampuni hiyo inategemea kwamba mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu safari hizo zitakuwa zimeshaanza.

Awamu hii pia inahusisha ununuzi wa ndege ambapo katika awamu ya kwanza tuliona ndege kama vile Bombardier na Boeing zilinunuliwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za kampuni lakini katika awamu hii zimeongezwa ndege mbili aina ya  Airbus ambapo moja iliwasili nchini tarehe 23 Disemba mwaka 2018 na nyingine inatarajiwa kuwasili Januari 11 mwaka huu na  mwisho wa mwaka huu Kampuni hiyo inatarajia kupokea ndege nyingine.

Upanuzi huu pia unahusisha kuongeza wafanyakazi ambapo katika awamu hii pia kampuni imeongeza wafanyakazi na wahudumu mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma kwa sababu unapoongeza safari kunakuwa na mahitaji mengi ya watoa huduma.

Faida zilizopatikana kutokana na upanuzi wa huduma za ATCL

Faida ziko nyingi kwa kampuni, miongoni mwa faida hizo ni pamoja na;

Kurudisha imani kwa wateja wake ambapo watu wanaiamini na wanaendelea kuiamini ATCL kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika, hii ni kutokana kwamba huduma zake zimekuwa za uhakika na zinapatikana sehemu nyingi kwa sababu kuna vifaa pamoja na watoa huduma wa kutosha.

Kampuni imeweza kuwapa watu uwezo wa kusafiri kwa kutumia usafiri wa anga, hii ni faida kwa sababu watu walikuwa wana uhitaji mkubwa wa usafiri wa anga ambao unaweza kukidhi mahitaji yao  na ATCL imeweza kulifanikisha hilo.

Kuongezeka kwa abiria ambao wanatumia ndege za ATCL kutoka abiria chini ya 4,000 kwa mwezi hapo awali mpaka kufikia abiria zaidi ya 40,000 hivi sasa.

Kitu kingine ni kuongezeka kwa mapato kwa sababu hapo awali mapato ya kampuni kwa mwezi yalikua chini ukilinganisha na sasa, hivyo hii pia ni moja ya faida iliyotokana na upanuzi wa huduma za kampuni hiyo.

Faida nyingine ni kuweza kuchangia katika pato la taifa, kupanua wigo wa shughuli za kitalii, kuongeza idadi ya wawekezaji wanaokuja hapa nchini, kuwawezesha watanzania kufanya biashara zao nje na ndani ya Tanzania pamoja na kutoa ajira kwa watanzania.

Kingine ambacho kampuni inajivunia ni kuweza kukabiliana na ushindani katika soko hapa nchini kutokana na kujiimarisha kihuduma. Hii imetokana na kujipanua katika utoaji wa huduma zake kama vile ununuzi wa ndege kubwa na za kisasa, kuongeza safari, kuongeza wahuduma, wafanyakazi nk.

Hii pia imesababisha ATCL kuongeza asilimia za umiliki wa soko (Market Share) kutoka asilimi 2.5% hapo awali mpaka kufikia asilimia 31%. Hivyo mbali na kukabiliana na ushindani pia kampuni hiyo imeongeza ushindani katika soko……..itaendelea wiki ijayo.