Ifahamu Airbus A220-300 ndege itakayotumika kwa safari za Harare na Lusaka

Jafari Juma, Mwananchi

Ndege mpya ya sita ambayo imekuwa ya karibuni zaidi kununuliwa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kutumiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) iliwasili jijini Dar es Salaam January 11 mwaka huu. Ndege hiyo ambayo imetengenezwa na Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus, ni ya muundo wa A220-300.

Ndege za Airbus A220 zilikuwa zinafahamika kama Bombardier CS100s hapo awali kabla ya Kampuni ya Airbus kununua mradi huo wa utengenezaji wa ndege za C Series.

Ununuzi huo ulifanikishwa kupitia mkataba wa kibiashara kati ya Kampuni ya Airbus na Kampuni nyingine mbili ambazo ni; Bombardier Inc. na Investissement Québec ambao ulianza kutekelezwa 1 Julai, 2018.

Airbus sasa inamiliki asilimia 50.01% ya hisa katika ubia wa utengezezaji wa ndege hizo ambao kirasmi hufahamika kama C Series Aircraft Limited Partnership, huku Bombardier ikimiliki asilimia 34% na Investissement Québec wakimiliki takribani  asilimia  16% ya hisa.

Makao makuu ya mradi huo wa utengenezaji wa ndege pamoja na karakana zake vinapatikana Mirabel, Québec. Kutokana na ushirikiano huo, Airbus inamiliki hisa nyingi, hivyo mradi wa C Series unahesabiwa kuwa chini ya Airbus kwa sasa.

Safari za ndege za Kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Lusaka na Harare zitakua safari za moja kwa moja kwa kutumia ndege mpya ya Airbus A220-300 yenye uwezo wa kuchukua abiria 132.

Ndege hiyo inabeba abiria 12 kwa upande wa daraja la biashara (Business Class) na abiria 120 kwa daraja la kawaida (Economy). A220-300 inao uwezo wa kubeba mizigo mpaka tani 4 kwa wakati mmoja ikiwa na biria. Ndege hii ina uwezo wa kuruka angani kwa umbali wa futi 41,000 kutoka usawa wa bahari.

Ndege hii urefu wake ni mita 38.7, na kwa jumla inaweza kuketi abiria 141 ambapo kati ya hao abiria 12 kwa upande wa daraja la biashara (Business Class) na abiria 120 kwa daraja la kawaida (Economy).

Urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5, na upana wa mabawa yake ni mita 35.1.

Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa 5,920km safari moja, na inaweza kupaa ikiwa na uzani wa tani 67.6, na kutua ikiwa na uzani wa tani 58.7.

A220-300 ndiyo ndege kubwa miongoni mwa ndege za familia ya A220 na iliundwa kulenga soko la safai za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.

Ni ndege ambayo imeundwa kupunguza gharama ya matumizi ya mafuta kwa kila safari na pia kuwa yenye uwezo wa juu.

Injini zake zimepunguza matumizi ya mafuta kwa kila abiria kwa asilimia 20 ukilinganisha na ndege za awali za aina yake.

Ndege za A220 zimejengwa kwa vipande vinavyoweza kutengenezwa kwa haraka kiwandani iwapo vitahitajika wakati wa ukarabati.

Injini zake pia huwa za familia moja. Marubani waliozoea ndege aina ya A220-300 na A220-100 hawahitaji mafunzo zaidi kuweza kuziendesha.

Mbali na Safari za Harare za Lusaka ambazo zinatarajiwa kuanza February 22 Februari mwaka huu, ATCL ianatarajia kuanza safari za Johannesburg (Afrika Kusini), Mumbai (India), Hong Kong, Thailand pamoja na Guangzhou (China) ambazo zinatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha Machi mpaka Juni 2019.

Aidha, kutokana na ujio wa ndege hizi kwa sasa Kampuni ya ndege Tanzania ina jumla ya ndege saba, baada ya kununuliwa ndege sita chini ya mpango wa kufufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.

Kuna Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Juni 2017; Bombardier CS300 mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua Tanzania kati ya mei na Julai 2018. Kampuni hiyo ilikuwa na Bombardier DASH8 Q300 moja ambayo ilikuwa ikihudumu tangu 2011.

ATCL inaendelea kuwakaribisha wafanyabiashara na wananchi kufurahia huduma bora za safari za ndege ambazo zina viwango vya kimataifa. ATCL iko vizuri na imejipanga kuwahudumia.